Serikali imesema itaendelea kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO), ili kuharakisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa wananchi.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Godwin Mollel, aliyasema hayo juzi jijini Dar es Salaam katika mkutano na kikao kazi kati ya serikali na mashirika hayo.

Alisema serikali inatambua mchango wa mashirika hayo nchini katika kuleta maendeleo huku akiyahakikishia kuyapa ushirikiano.

“Serikali inatambua mchango wa NGO, hivyo niwahakikishie serikali ipo tayari kuendelea kushirikiana nanyi,” alisema Dk. Mollel.

Kadhalika, Dk. Mollel aliwataka viongozi walioko katika ngazi za mikoa nchini kubainisha shughuli zinazofanywa na mashirika hayo, ili kuyatambua na kuongeza uwajibikaji.

Katibu Mkuu wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo Yakiserikali (NaCoNGO), Focus Magwesela, alisema hadi Januari 17 mwaka huu, jumla ya NGO 11,089 zilikuwa zimesajiliwa.

Magwesela alisema kati ya mashirika hayo, 326 ni ya kimataifa na ya ndani 8,622, huku 672 yakisajiliwa kwenye mikoa na ngazi ya wilaya ni 1,099.

"NGO tunapendekeza vibali vihamishiwe kwa maofisa kutoka ofisi za ustawi badala ya kuwa Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Kwa kuwa wakati mwingine vibali vinakwamisha utendaji kazi wa mashirika,” alisema Magwesela.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Foundation for Civil Society (FCS), Francis Kiwanga, alisema kikao hicho kimetoa njia na mwongozo katika kuboresha utendaji kazi na majukumu wa mashirika hayo.

“Tumekubaliana na serikali kuwa na mkutano kila mwaka, ili kupitia kanuni ambazo hazitekelezeki, hazizingatiwi na kubadilishwa.”

Alisema matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa mashirika hayo pamoja na serikali yakiboreshwa, yatasaidia mashirika hayo kutochukua muda mwingi kusafiri umbali mrefu ili kuandaa taarifa za utendaji kazi na kuwasilisha serikalini.

“Serikal ikitumia TEHAMA itapunguza gharama na mfumo wa kutumia makaratasi kuandaa ripoti, mfumo ambao hupoteza muda,"alisema Kiwanga.

Mkutano huo ulikutanisha washiriki wapatao 300, ikiwamo mashirika ya ndani na kimataifa, ulilenga kutoa fursa kwa wadau wa sekta tofauti, kutambua mchango wa NGO, kutoa mapendekezo ya marekebisho ya sera, kanuni na sheria ambazo zinazosimamiwa na kuratibiwa na mamlaka.