Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya kiserikali (NACONGO) limetangaza kuanza mchakato wa mapitio na maboresho ya kanuni zake ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo na ushauri wa bodi ya uratibu wa mashirika yasiyo ya kiserikali kwa Baraza hilo yaliyotolewa mwezi Disemba mwaka jana.

Kanuni hizo zinazofanyiwa marekebisho ni pamoja na Kanuni za uendeshaji wa Baraza na Kanuni za Uchaguzi wa Baraza ambazo zimetungwa chini ya sheria ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali namba 24 ya mwaka 2002.

Akizumgumza na vyombo vya habari Katika Ofisi za NaCONGO Jijini Dar es salaam, Kaimu Katibu Mkuu Focus Magwesela amesema mapitio ya kanuni hizo yameshaanza na zoezi la uchambuzi wa kanuni ili kubaini maeneo ya kufanyiwa marekebisho.

"Baada ya uchambuzi, hatua inayofuata ni kupata maoni ya wadau wa sekta juu ya mchakato kwa kujaza madodoso na kufanya mazungumzo na mtaalamu mwelekezi ili kupata maoni ya awali ya wadau," amesema Magwesela.

Mapitio ya kanuni hizo yanalenga kubaini changamoto za ndani na nje zinazokabili uendeshwaji wa shughuli mbalimbali za baraza na kutengeneza mkakati wa kuzitatua, kupitia kanuni za uendeshaji wa baraza zikiwemo kanuni za Uchaguzi na kuzifanyia marekebisho pamoja na kufanya uchaguzi Mkuu wa Baraza hilo

"Waraka huu unalenga kuwataarifu wadau juu ya utekelezaji wa kifungu cha pili cha maelekezo yaliyopo ambao ulianza Juni 15 mwaka huu, na unatarajiwa kukamilika septemba 30 mwaka huu,"amesema Magwesela.

Aidha NaCONGO imetoa rai kwa wadau wa mashirika yasiyo ya kiserikali kushiriki Katika mchakato huo kwa Kutoa maoni yao juu ya dodoso na rasimu zitakazoandiwa na Baraza hilo.

Kwa upande mwingine NaCONGO limeyataka mashirika yasiyo ya kiserikali kutojihusisha Katika kushabikia, kusaidia au kuegemea upande wa chama chochote Cha kisiasa Wakati huu ambapo Tanzania inaelekea Katika uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Octoba, 2020.